OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI YAHIMIZA USHIRIKIANO NA WADAU


Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Gerson Mdemu akitoa maelezo wakati wa Mkutano wa Kazi kati ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wadau ( hawapo pichani)kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali zilizopo Mkoani Tabora ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma. Madhumuni ya Kikao kazi hicho ilikuwa ni kukutana wa wadau hao kwa lengo la kujadiliana, kubadilishana mawazo na kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali ambazo wadau hao pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wanakumbana nazo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Wadau walioshiriki kikao hicho ni kutoka Mahakama, Takukuru, Magereza, Polisi, Wakala wa Barabara, Maliasili, Halmashauri, Mawakili wa Serikali, Wanasheria na wanajamii. Kushoto kwa Naibu Mwanasheria Mkuu Wakili Mfawidhierikali Kanda ya Tabora Bw. Jackson Bulashi na kulia ni Kamanda wa Takukuru Tabora Bw. Fidelis Kalungura.
Sehemu ya wadau ambao wamekuwa na mazungumzo na majadiliano na Ujumbe wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ulioongozwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Bw. Gerson Mdemu. Majadiliano hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Takukuru Mkoani Tabora siku ya Ijumaa ( June 16) ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Wadau kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Mahakama, Polisi, Takukuru, Maliasili, Magereza, Halmashauri, Wakala wa Barabara,Mawakili wa Serikali na Wanasheria wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha majadiliano baina ya wadau hao na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambapo wameazimia kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zilizoibuliwa katika kikao hicho na kisha kupeana mrejesho.

Na Maura Mwingira, Tabora 

Katika kuadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali leo ( Juni 16) imekutana na wadau mbalimbali mkoani Tabora kwa madhumuni ya kujadiliana na kubadilishana mawazo yenye lengo la kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbalimbali za kiutendaji.

Akitoa maelezo ya awali mbele ya wadau hao kutoka taasisi za serikali zinazofanya kazi kwa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Mdemu pamoja na mambo mengine amesisitiza haja na umuhimu kwa wadau hao pamoja na Ofisi yake kufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake kwa ukamilifu.

“ Nyinyi ni wadau wetu muhimu sana sana, ni kwa sababu hiyo, katika wiki hii ya maadhimisho ya Utumishi wa Umma tukaamua kuja Mkoani Tabora ili tukutane nanyi.

Ni tumie basi, kikao hiki cha kazi kusisitiza kwenu, haja na umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano na ukaribu ili kwa pamoja tuisaidie na kuiwezesha Serikali itekeleze majukumu yake kwa ukamilifu”. Akasema Naibu Mwanasheria Mkuu.

Akaongeza kwamba, ni kwa kushirikiana na kufanya kazi kwa karibu licha ya kwamba kutaisaidia serikali lakini kubwa zaidi kutapuguza lawama na kunyosheana vidole.

“ Ni vema tutambue kuwa hakuna Taasisi ambayo inaweza kutekeleza majukumu yake pasipo kushirikiana na Taasisi nyingine. Lakini hili halilengi au haina maana ya kuingilia majukumu ya Taasisi au Mihimili mingine bali ni katika kutekeleza misingi na maadili ya utumishi wa umma” akabainisha Bw. Mdemu.

Wadau waliohudhuria majadiliano hayo ni kutoka Jeshi la Polisi, Mahakama, Magereza, Takukuru, Halmashauri, Wakala wa Barabara, na Idara ya Misitu na jamii. Akifafanua ziaidi hoja hiyo ya ushirikiano. Naibu Mwanasheria Mkuu ambaye ameambata na Wakurugenzi kutoka Divisheni zinazounda Ofisi ya Mwanasheria Mkuu. Pia amewataka wadau hao kuelezea kwa uwazi ni ushauri wa aina gani na katika eneo gani ambao wanauomba kutoka Ofisi ya Mwanasheria mkuu.

“Pale mnapoleta mikataba yenu katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwa ushauri au maoni, ni muhimu sana mkaweka wazi katika barua zenu ni maeneo gani gani ya mkataba mnayotaka ushauri au maoni, na kwa sababu gani. Badala ya kuleta maelezo ya mstari mmoja kwamba mnataka ushauri”.

Kasisitiza “ Jukumu letu kuu na la msingi na ambalo limeainishwa katika Katiba ni kutoa ushauri wa kisheria kwa Serikali na wadau wengine. Lakini ili ushauri huo uweze kutolewa kwa ukamili,utaalamu na kwa mujibu wa sheria inayosimamia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu . Hivyo ni lazima basi wadau wetu wawe tayari kutoa ushirikiano kwa kuweka wazi maeneo wanayotaka kushauriwa. Tukifanya hivi tutakuwa tunaisaidia sana Serikali”.

Wakati huo huo Mwanasheria Mkuu wa Serikali amewashukuru wadau hao kwa kutenga muda wao na kuitikia wito wa kukutana na kubadilishana na mawazo ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wao wadau hao wameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuamua safari hii kukutana na wadau wa Mkoa wa Tabora na kwamba mikutano ya aina hiyo ni muhimu sana katika uboreshaji wa uhusiano, ushirikiano na utetekelezaji wa majukumu ya kila taasisi.

Wadau hao pamoja na kutoka maoni yao na michango yao pia wameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake ya utoaji wa ushauri kwa wakati.

Katika maadhimisho ya mwaka jana Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikutana na wadau wa Mkoa wa Dar Es Salaam.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment