MAMIA YA WANANCHI WAJITOKEZA KUJISAJILI VITAMBULISHO VYA TAIFA WILAYA YA MUFINDI
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi akizungumza jambo na Afisa Usajili Mkoa wa Iringa bwana George Mushi kabla ya kuanza zoezi la usajili wa Wananchi katika Kata za Ifwagi, Ikongosi na Ihalimba. 
Maafisa wa JKT na NIDA wakipokea maelekezo ya Mkuu wa Wilaya Mhe. Mhe. Jamhuri William kabla ya kuanza utekelezaji wa zoezi la Usajili 
Wananchi wakipokea maelekezo ya namna ya kushiriki zoezi la Usajili linaloendelea Wilayani Mufindi. 
Baadhi ya wananchi katika Kata ya Ifwagi wakiwa kwenye foleni kusajiliwa zoezi la Vitambulisho vya Taifa linaloendelea Wilayani Mufindi. 
Maafisa wa NIDA wakiendelea na zoezi la uchukuaji alama za Vidole, picha na saini ya Kielektroniki wakati wa zeozi la Usajili likiendelea kwa wananchi wa Wilaya ya Mufindi. 
Afisa Usajili mkoa wa Iringa bwana George Mushi akizungumza jambo na wananchi wa Kata ya Ikongosi wakati wakisubiri kupata huduma ya usajili vitambulisho vya Taifa (NIDA)

………………………….

Wananchi wa Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa wamejitokeza kwa wingi kusajili Vitambulisho vya Taifa kufuatia maelekezo ya Mkuu wa mkoa huo Mhe. Amina Masenza ambaye amejizatiti kuweka historia ya kuwa mkoa wa kwanza kwa wananchi wake kuwa na Vitambulisho vya Taifa; baada ya kufanikisha kwa asilimia kubwa zoezi la kuwasajili Watumishi wa Umma lililofanyika nchi nzima.

Kwa kuanza; zoezi la Usajili kwa mkoa wa Iringa limeanza katika Wilaya ya Mufindi ambapo zaidi ya wananchi 70,000 wameshajiliwa katika Kata 20 kati ya Kata 36 zilizopo Wilaya humo, huku wananchi 50,000 wakiwa tayari na Vitambulisho vya Taifa.

Akizungumza wakati wa kukagua utekelezaji wa zoezi hilo; Mkuu wa Wilaya ya Mufindi ambako zoezi hilo linaendelea kwa sasa Mhe. Mhe. Jamhuri William amesema “kama Wilaya wamejipanga kuhakikisha zoezi la kuwasajili wananchi linafanyika katika muda mfupi iwezekanavyo na kwamba uhamasishaji umefanyika kwa njia mbali mbali kuhakikisha wananchi wanatumia vema fursa Iliyopo”

Amesisitiza mbali na kuwasajili wananchi; Wilaya ya Mufundi pia inaendelea na zoezi la kuwasajili Wageni na Wakimbizi wanaoishi kihalali Wilayani humo, lengo likiwa ni kupata taarifa sahihi za watu na kuimarisha upatikanaji wa huduma kiurahisi kwa wananchi.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Amina Masenza alizindua kuanza kwa zoezi la usajili mkoa wa Iringa na kuelekeza kwa kushirikiana na NIDA kila Wilaya kuhakikisha ndani ya siku 60 kuwa wamekamilisha zoezi la kuwasajili wananchi Vitambulisho vya Taifa; na kuwahakikishia wananchi Ofisi yake itahakikisha wananchi wote wakaosajiliwa wanapata Vitambulisho vyao kwa wakati ili matumizi kuanza mara moja.

Tayari Mamlaka imeanza mipango ya kuunganisha watoa huduma mbalimbali kwenye mfumo, ili Vitambulisho vya Taifa kuanza kutumika katika huduma mbalimbali pamoja na kuimarisha ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Iringa.

Katika mkoa wa Iringa zoezi la kuwasajili wananchi limekuwa likifanywa kwa ushirikiano na kikosi cha JKT ambao wamepata mafunzo ya namna ya kuendesha zoezi la Upigaji picha na uchukuaii alama za kibaiolojia.

Ndg George Mushi Afisa Usajili mkoa wa Iringa; amesema kwa sasa zoezi linaloendelea lihahusu Kata za Ifwagi, ikongosi pamoja na Ihalimba.

“Wananchi wanaosajiliwa ni wale wote wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ikihusisha ujazaji fomu, uchukuaji alama za vidole, picha na saini ya Kielektroniki na uhakiki wa taarifa kwa kila mwombaji. NIDA imejipanga kuhakikisha katika kila hatua vitambulisho vinatolewa mapema iwezekavyo ili kuruhusu kuanza kwa matumizi ya Vitambulisho hivyo katika huduma mbalimbali” alisisitiza.

Nyaraka muhimu zinazohitajika katika kuthibitisha uraia, umri na makazi ya mwombaji ni pamoja na Cheti cha Kuzaliwa, Vyeti vya Shule ya Msingi na Sekondari, Elimu ya Juu, Leseni ya Udereva, Kadi ya Mpiga kura, Kitambulisho vya Bima ya Afya, Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi, pamoja na pasi ya kusafiria (Passport).
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment