WAAJIRI WATAKIWA KUWASILISHA MAFAO YA FIDIA YA WAFANYAKAZI WAO KWA WAKATI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira na wenye ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama, akikata utepe kuzindua rasmi utoaji wa Fidia kwa Wafanyakazi waliopatwa na madhara ya kiafya mahali pa kazini. Uzinduzi huo ulifanywa na Waziri Mhagama kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dar es Salaam, Desemba 20, 2016. Wengine pichani ni Manaibu wakeKulia kwake ni Naibu wake, Dkt. Abdallah Possi na Mh. Anthony Mavunde, Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini ya WCF, Emmanuel Humba, (wane kulia), na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Masha Mshomba.( Picha na Muhidin Sufiani) 
Na Muhidin Sufiani, Dar

SERIKALI imewaagiza Waajiri wote nchini kuwasilisha kwa wakati michango ya mafao ya fidia kwa wafanyakazi ili kuwawezesha watumishi wao kupata huduma za matibabu pindi watakapoumia au kuugua wakiwa katika maeneo yao ya kazi.

Agizo hilo limetolewa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Ulemavu) Jenister Mhagama wakati alipokuwa akizindua huduma za utoaji wa mafao ya fidia na ubia baina ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi (WCF) na watoa huduma za afya nchini.

Mhagama alisema suala la uchangiaji wa mafao hayo sio la hiari ila lipo kisheria na hivyo ni wajibu wa waajiri wote nchini kuhakikisha kuwa wafanyakazi wao wanaingizwa katika mfumo huo ili kuwawezesha wafanyakazi kuwa na uhakika wa kulipwa fidia pindi wanapokuwa kazini.

“Katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imelipa michango yote ya wafanyakazi wake, na huu ni mfano unaopaswa kuigwa na waajiri wengine nchini, na natoa rai kwa Chama cha Waajiri Nchini (ATE) na Shirikisho la Wafanyakazi nchini (TUCTA) linasimamia suala hili” alisema Mhagama.

Aidha Mhagama alisema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo wa wafanyakazi nchini ni kusaidia kutatua kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi, ambao wamekuwa wakilalamikia huduma hafifu zinazotolewa pindi wapatapo majanga mbalimbali wakiwa kazini ikiwemo ajali na vifo.

Waziri Mhagama alitaka Bodi ya mfuko huo kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria zilizopo ili kuhakikisha kuwa waajiri wote hususani wa sekta binafsi wanawasilisha michango kwa wakati.

Akifafanua zaidi Waziri Mhagama aliuataka mfuko huo kujitangaza zaidi kwa sekta zisizo rasmi ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi hususani wa kipato cha chini kujiunga na mfuko huo na kuwasaidia kufaidi huduma zinazotolewa.

“Natoa rai kwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini ikiwemo wa WCF mjitangaze katika sekta zisizo rasmi ikiwemo waendesha bodaboda, akina mama lishe, kwa kuwa idadi yao ni kubwa na hiyo itawezesha kupata wanachama wengi zaidi” alisema Mhagama.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Musomba alisema hadi kufikia sasa mfuko huo umeweza kutoa usajili wa waajiri 5945 pamoja na kuendesha mafunzo mbalimbali ya kuwajengea uwezo watumishi wa mfuko huo ikiwemo madaktari.

Aidha Musomba anasema pia mfuko huo umeingia ubia na taasisi 7 za utoaji huduma za afya nchini, ambazo ni Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), na Taasisi ya Kansa ya Ocean Road.

Musomba anazitaja taasisi nyingine kuwa ni Strategis, AAR, mfuko wa Jubilee, na Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo taasisi hizo zinazoendelea kushughulikia kesi 189 zilizolipotiwa katika mfuko huo.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Aggrey Mwinuka alisema mfumo huo wa fidia umekuja katika wakati muafaka kwa kuwa sheria zilikuwepo katika vitabu na hazikuwa na utekelezaji uliokusudiwa.

Mwinuka alisema ili kuhakikisha kuwa malengo ya mfuko huo yanatekezeka ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa inafanya majadiliano ya mara kwa mara na waajiri ili kuangalia viwango vya makato ya michango ya wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi.

Mwenyekiti wa Bodi ya mfuko huo, Emmanuel Homba alisema uwekaji wa mfumo wa mafao ya fidia utawezesha wafanyakazi katika sekta za umma na binafsi kuchangia kikamilifu katika Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.
Waziri Mhagama akihutubia.
Mwenyekiti wa bodi ya WCF, Bw. Emmanuekl Humba akitoa hotuba yake 
Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw.Masha Mshomba, akitioa hotuba yake.
Mgeni rasmi, manaibu waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, viongozi wa WCF, na waliotunukiwa vyeti wakiwa kwenye bpicha ya pamoja.
Waziri Mhagama, akimkabidhi Cheti cha utoaji huduma bora za afya, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bernard Konga, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Huduma ya Utoaji wa Mafao ya Fidia kwa Wafanyakazi na Ubia kati ya Mfuko na watoa huduma za afya, WCF uliozinduliwa jijini Dar es Salaam, leo. 
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge, Mhe. Jenista Mhagama, akimkabidhi Cheti cha utoaji huduma bora za afya, Mkurugenzi Mtendaji wa ‘Muhimbili Orthopaedic Institute’ Dkt. Othman Kiloloma, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Huduma ya Utoaji wa Mafao ya Fidia kwa Wafanyakazi na Ubia kati ya Mfuko na watoa huduma za afya, WCF uliozinduliwa jijini Dar es Salaam, leo.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment