TUMIENI FURSA ZILIZOPO KUIFANYA SEKTA YA FILAMU KUWA CHACHU YA MAENDELEO NCHINI – BIBI. MILLAO


  Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao (kulia) akizungumza na washiriki (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. Kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo.
 Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo (katikati) akifafanua jambo wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao na kushoto ni Rais wa Shirikisho la Filamu Bw. Simon Mwakifwamba.
 Kaimu Afisa Utamaduni Mkoa wa Mara Bw. Sheikhdadi Said (kulia) akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. Katikati ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao na Kushoto ni Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo.
 Katibu wa chama cha waigizaji Mkoa wa Mara Bw. Jonson Bambai (aliyesimama) akichangia mada wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara. 
 Mtoa mada kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Bw. Richard Ndunguru akitoa mada ya uandishi wa miswada ya filamu na utafiti kwa wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza wakati wa ufunguzi wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau hao leo Mkoani Mara. 
Baadhi ya wadau wa sekta ya filamu na michezo ya kuigiza kutoa mkoa wa Mara wakifuatilia kwa makini mada zilizokua zikiendelea wakati wa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara.Picha na: Genofeva Matemu – WHUSM, Mara


Na Genofeva Matemu – WHUSM.

Wanatasnia wa filamu nchini wametakiwa kutumia fursa zilizopo kikamilifu ili kuifanya sekta ya filamu kuwa chachu ya maendeleo ya nchi na kuleta ushindani wa kazi za filamu zinazozingatia  ubobezi na hatimaye kuingia katika soko la ushindani. 

Rai hiyo imetolewa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi. Nuru Millao wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza leo Mkoani Mara.

“Nimatumaini yangu kuwa mafunzo mnayoyapata hapa yakijumuishwa na fursa mlizonazo za mandhari mahususi ya upigaji picha katika Mkoa wetu wa Mara, maeneo mazuri na asilia ya kitalii, utamaduni wetu, maliasili, lugha ya kiswahili na mambo mengine mengi mkiyazingatia katika uandaaji wa filamu zenu hakika ushindani wa filamu zetu utakuwa mkubwa sana” amesema Bibi. Millao.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Bibi. Joyce Fissoo amesema kuwa Lengo la warsha hiyo ni kuhakikisha kuwa wadau wanazalisha kazi bora na hatimaye wanapata mrejesho stahiki kutokana na kazi zao hivyo wadau walioshiriki warsha watumie fursa waliyoipata kwani warsha imezingatia ushirikishwaji wa hali ya juu kwa kuwapa wadau fursa ya kuchagia na kujadiliana.

 “Azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa la viwanda hivyo kwa mantiki hiyo, katika warsha hii suala la namna gani tasnia iimarishwe ikiwa ni pamoja na uwepo wa viwanda vya filamu litatiliwa mkazo kutokana na hali ya Sekta ya Filamu kuendelea kuimarika kutokana na jitihada za wadau kwa kushirikiana na Serikali” amesema Bibi. Fissoo.

Naye Katibu wa chama cha waigizaji Mkoa wa Mara Bw. Jonson Bambai amesema kuwa warsha ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wadau wa Sekta ya filamu na michezo ya kuigiza ni nembo tosha kwa waigizaji wa mkoa wa Mara kwani itawawezesha kuandaa filamu zitakazowavutia watazamaji kutoka mwanzo hadi mwisho wa filamu kwa kutumia fursa zilizopo katika mkoa wa mara na kutangaza upekee wa kabila la wakurya ndani na nje ya nchi.

Tasnia ya filamu imeendelea kuwa chombo muhimu sana kinachochangia katika Maendeleo ya Taifa. Sote tutakubaliana kuwa ile dhana ya awali kuwa filamu ni chombo cha kutoa burudani tu imeanza kufutika kufuatia sekta hii kutoa ajira kwa makundi mbalimbali na kuchangia katika uchumi wa nchi. 
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment