Donald Trump kulipwa $1 kila mwaka

Rais mteule Donald Trump amesema hatapokea mshahara wa rais wa $400,000 (£319,500) kila mwaka

Image copyrightGETTY IMAGES
Image captionRais mteule Donald Trump amesema hatapokea mshahara wa rais wa $400,000 (£319,500) kila mwaka

Donald Trump kulipwa $1 kila mwaka

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema hataki kulipwa mshahara wa rais wa $400,000 atakapochukua hatamu Januari mwakani. Badala yake atakuwa akilipwa $1 pekee kila mwaka.
Alifichua mpango wake huo wakati wa mahojiano na Lesley Stahl kipindi cha 60 Minutes cha CBS News.
Ingawa hakujua rais huwa analipwa pesa ngapi, Bw Trump alisema alidhani anahitaji kuchukua tu $1.
Baada ya Bi Stahl kumjulisha kwamba mshahara wa rais ni $400,000, alisema: "Hapana, sitaupokea mshahara huo. Sizichukui kamwe."
Rais huyo mteule anatimiza ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni.
Aliambia waliohudhura mkutano wake Septemba kwamba mshahara wa rais si jambo kubwa kwake.

Kuna viongozi wengine walioukataa mshahara?
Bw Trump si kiongozi wa kwanza wa Marekani kukataa mshahara.
Herbert Hoover, aliyekuwa ametajirika kupitia biashara ya madini kabla ya kuingia madarakani, na John F Kennedy, aliyerithi utajiri mwingi, wote walikataa kupokea mashahara na badala yake wakatoa pesa hizo zisaidie wasiojiweza katika jamii.
John F Kennedy, picha iliyopigwa 23 Oktoba 1962Image copyrightPA
Image captionJFK alitoka familia ya viongozi mashuhuri karne ya 20 nchini Marekani
Meya wa zamani Michael Bloomberg, gavana wa zamani wa California Arnold Schwarzenegger na gavana wa zamani wa Massachusetts Mitt Romney pia walikataa kupokea mishahara yao.
Mark Zuckerberg, mwanzilishi wa mtandao wa kijamii wa Facebook, ndiye mfanyakazi anayelipwa mshahara wa chini zaidi katika kampuni hiyo.
Aidha, ni miongoni wa CEO (Afisa Mkuu Mtendaji) wengi ambao hulipwa mshahara wa $1 pekee.
Sergey Brin na Larry Page wa Google pia wamekuwa wakilipwa $1 kwa mwongo mmoja sasa.
Larry Ellison wa Oracle pia aliukataa mshahara wake kwa miaka kadha alipokuwa CEO. Afisa mkuu mtendaji wa Hewlett Packard Enterprise (HP) Meg Whitman apia alichukua hatua sawa.
Viongozi hawa hata hivyo hujipatia pesa kupitia njia nyingine. Wengi ni kupitia hisa wanazomiliki na wengine hulipwa kwa kutegemea matokeo au mapato ya kampuni.

Viongozi wa nchi nyingine hulipwa pesa ngapi?
Licha ya $400,000, anazolipwa rais wa Marekani, pia hupewa jumla ya $50,000 ambazo huwa hazitozwi ushuru, kwa mujibu wa sheria.
Waziri mkuu wa Canada alilipwa C$340,800 (£201,202) mwaka uliopita.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alilipwa $242,000 (£193,976) naye Rais wa Ufaransa Francois Hollande akalipwa $198,700 (£158,000), kwa mujbiu wa taarifa ya CNN ya mwezi Agosti.
Bw Hollande alipunguza mashahara wake kwa 30% alipoingia madarakani mwaka 2012.
Theresa MayImage copyrightREUTERS
Image captionWaziri Mkuu wa Uingereza Theresa May hulipwa $186,119 (£143,462)
Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May hulipwa $186,119 (£143,462) kila mwaka, ingawa thamani yake kwa dola imeshuka baada ya Uingereza kupiga kura kujiondoa EU.
Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza David Cameron alishutumiwa sana alipoongeza mshahara wake kwa 10% mwaka 2015.
Hata hivyo alisema jambo la busara ni kulipwa "mshahara unaolingana na kazi".
Aliongeza kwamba kuongezewa mashahara kulimpa uwezo zaidi wa kutoa pesa za hisani na mambo mengine ya kusaidia jamii.

Wazo hili lilitoka wapi?
Mwanzilishi wa Apple Steve Jobs alivumisha wazo la mshahara wa $1 Silicon Valley baada yake kurejea katika kampuni hiyo 1997.
Wakuu wa kampuni mbalimbali wamekuwa wakikosa kupokea mishahara yao tangu Vita Vikuu vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.
Steve Jobs mwaka 2011Image copyrightJUSTIN SULLIVAN
Image captionMwasisi wa Apple Steve Jobs ndiye aliyepatia umaarufu wazo la mshahara wa $1
Wakuu wa kampuni, benki na viwanda mbali ambao walijitolea kutumikia nchi katika majukumu mbalimbali wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia walifahamika kama "wanaume wa dola moja kila mwaka". Kwa kuwa sheria nchini Marekani huharamisha mtu kufanya kazi bila kulipwa, viongozi hao walipokea mshahara wa $1 kutimiza matakwa ya sheria kwamba walikuwa wanalipwa.
Wazo hilo lilirejea wakati wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia ambapo wakuu wa kampuni kubwa kama vile Lockheed, Chrysler na Boeing walijitokeza kutumikia nchi kama uzalendo.

Donald Trump atapata pesa wapi?
Ana biashara nyingi ambazo zinampa pesa, ingawa kwa baadhi watu wameuliza maswali. Alitangaza majuzi kwamba wanawe - Donald Jr, Eric, na Ivanka - na mume wa Ivanka, Jared Kushner, watakuwa kwenye kamati inayosimamia mpito.
Bw Trump hatakiwi kuuza mali yake, ambayo thamani yake inafikia mabilioni, lakini amesema biashara zake zitasimamiwa na watoto wake.
Lakini kuhusika kwa watoto wake katika shughuli ya mpito kumewafanya baadhi kusema kutakuwa na mgongano wa maslahi.
Isitoshe, Bw Trump bado hajatoa taarifa zake za kodi na hakuna ajuaye iwapo kuna watu kutoka nje wanaomiliki sehemu ya hisa aktika biashara zake. Hilo linaweza kuathiri uhusiano wa Marekani na nchi za nje, hivyo kuibua suala la mgongano wa maslahi.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment