Ziara ya Mfalme wa Moroco ni Fursa kwa Wafanyabiashara

Immaculata Makilika- MAELEZO 

Ziara ya Mfalme wa Moroco ni Fursa kwa Wafanyabiashara


Moroco ni nchi iliyopo Kaskazini Magharibi mwa Afrika, ambayo imepakana na bahari za Atlantiki na Mediteraniani, na upande wa bara imepakana na nchi za Algeria, Mauritania.mpaka wa kusini unatajwa kuwa Sahara Magharibi.

Nchi ya Moroko inakadiriwa kuwa na eneo la Km2 446,550, huku sehemu kubwa ikiwa ni jangwa la Sahara na watu wengi nchini humo huishi kwenye sehemu zilizo na rutuba hasa karibu na maeneo ya pwani.

Nchi hiyo ina milima inayofunika eneo kubwa, ikiwemo milima ya Atlas ambayo ipo katikati ya nchi hiyo kutoka kusini magharibi kuelekea upande wa kaskazini mashariki na mji mkuu wake ukiwa ni Rabat wenye wakazi milioni 2, aidha mji mkubwa ni Casablanka.

Nchi ya Moroco ilipata uhuru wake mwaka 1956 kutoka kwa nchi za Ufaransa na Hispania zilizokuwa zikiitawala, na kikatiba inaongozwa na Mfalme, kwa sasa inaongozwa na mfalme anayeitwa Mohammed wa VI, na Waziri Mkuu ni Abdelilah Benkirane. Watu wa Moroko hutumia lugha rasmi za kiarabu na kiberiberi. Fedha yao inajulikana kama Dirham, zaidi ya 90% ya watu wake ni waislamu. Uchumi wa Moroco unategemea zaidi utalii, sekta ya mawasiliano, viwanda vya nguo pamoja na kilimo.

Hivi karibuni, kwa mara ya kwanza tunashuhudia ziara ya Mfalme wa Moroco Mohammed wa VI aliyewasili nchini wiki hii kwa ziara ya siku tatu hadi Oktoba 25 mwaka huu. Ujio wa Mfalme huyo wa Moroko unaidhihirishia dunia kwa kiasi gani diplomasia ya Tanzania imeendelea kukua kwa kasi, ikiwa ni sambamba na kukuza diplomasia ya uchumi.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga anasema kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza uhusiano wa kati ya Tanzania na Moroco hususani katika masuala ya uchumi na biashara kwa faida ya watu wa nchi hizi mbili. “ Ziara hii imejikita zaidi katika kukuza ushirikiano wa kiuchumi na biashara, ikizingatiwa kuwa nchi ya Moroco imefanikiwa katika nyanja mbalimbali kama vile miundombinu, afya, madini na ulinzi”.

“Vile vile wafanyabiashara kutoka Moroko watafanya mazungumzo na wa hapa nchini kwa lengo la kubadilishana uzoefu na ni hatua nzuri itakayoweza itakuza uhusiano wetu pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi” anasema Balozi Mahiga. Maroko imepiga hatua katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, uvuvi ,viwanda, kilimo na madini.

Mambo yaliyopo katika mpango huo ni pamoja na maboresho ya reli, na barabara, kuboresha viwanja vya ndege kwa viwango vya kimataifa ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya ndege zinazoingia Moroco. Sambamba na hilo bandari maarufu zimeandaa utaratibu wa safari za kitalii.

Vitu na Maeneo mbalimbali yamekuwa sehemu ya kuvutia utalii kutoka nchi za Ujerumani, Ufaransa, na Hispania, ambapo huvutiwa na fukwe za bahari,milima ya Atlas, pamoja na miji maarufu ya kama ya Tangie, Marrakech, Casablanka na Tarfaya. Sekta ya madini ni sekta muhimu kwa vile inachangia uchumi wa nchi kwa asilimia 6 ya pato la ndani la taifa na asilimia 35 ya pato la kigeni kwa nchi ya Moroco.

Ili kukuza sekta ya utalii nchini humo, matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameimarishwa na kuweza kutangaza vivutio mbalimbali kwa kuhususha sekta binafsi katika kutangaza utalii wa ndani, na kati ya nchi zilizofanikiwa katika hilo ni pamoja na nchi ya Malaysia ambapo mwaka 2011 ilipata watalii milioni 24.7 na mwaka 2012 ilipata watalii milioni 25 kutokana na matumizi ya TEHAMA.

Jitihada mbalimbali zimefanyika katika kusaidia sekta ya utalii nchini kukua na kuchangia zaidi pato la taifa, ambapo kupitia maboresho kuongeza ndege zenye safari ya moja kwa moja hadi nchini, na kuboresha miundombinu ya barabara sekta hiyo imeweza kupata mafanikio.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment