JAMII ZA WAKULIMA NA WAFUGAJI WILAYANI KILOSA ZATAKIWA KUISHI KWA AMANI - MAKAMBA


Na Lulu Mussa, Morogoro

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba ameitaka jamii ya watu wa Parakuyo katika Wilaya ya Kilosa kuishi kwa amani, uvumilivu na upendo miongoni mwao kwani ndio misingi ya watanzania.

Rai hiyo imetolewa leo katika Mkutano wa hadhara uliojumuisha jamii za wakulima na wafugaji ambazo zimekuwa na migogoro ya mara kwa mara. Waziri Makamba alizitaka jamii hizo kuishi kwa amani na kuhifadhi mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.

Miongoni mwa changamoto zilizobainishwa na jamii hiyo ni kutokuwa na elimu juu ya mabadiliko ya Tabianchi na athari zake pamoja na kutokuwepo na matumizi bora ya ardhi.

Waziri Makamba ameuagiza uongozi wa Wilaya na Kijiji kushirikiana pamoja kuunda kamati ya 'Amani' itakayokuwa na wajumbe kutoka pande zote mbili za wakulima na wafugaji na viongozi wa madhehebu ya dini ili kutafuta suluhu ya kudumu baina ya pande mbili ambazo zimekua na migogoro ya mara kwa mara.

"Undeni Kamati hii mapema na Ofisi yangu itagharamia mafunzo kwa Kamati husika juu ya namna bora ya kutatua migogoro" alisisitiza Waziri Makamba.

katika jitihada za kukuza uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto zake, Waziri Makamba ameitaka Serikali ya Kijiji kuunda Kamati ndogondogo za Mazingira ambazo zipo kwa mujibu wa sheria ya Mazingira na kuahidi kuipati mafunzo Kamati hizo ikiwa ni pamoja na kutengeneza sheria ndogo ndogo zitakazotumika kama nyenzo ya kuhifadhi na kusimamia Mazingira ya maeneo yao.

Aidha, Waziri Makamba amesema kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ni muhimu sana na kuitaka jamii ya Parakuyo na Twa twa twa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhakiki na kuhesabu mifugo yako ili kubaini ni ardhi kiasi gani inahitajika kwa wakulima na kiasi gani kwa wafugaji. "ndugu zangu niwasihi, Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kuna kuwa na matumizi bora ya ardhi, hivyo nawashauri mmshiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kupata uwiano wa idadi ya mifugo na ardhi iliyopo" Makamba aliongezea.

Awali katika ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Morogoro Waziri Makamba pia alitembelea chanzo cha maji na kujionea changamoto za kimazingira katika mto Mambogo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe. Waziri Makamba yuko Mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba, wa tatu kutoka kulia akiangalia chanzo cha maji kilichovamiwa katika Mto Mambogo.
Wananchi wa Kijiji cha Parakuyo wakisalimiana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba kabla ya kufanya mkutano wa hadhara kijijini hapo.
Sehemu ya Wananchi wa waliojitokeza katika Mkutano wa hadhara katika kijiji cha Parakuyo Wilayani Kilosa. Wananchi hao walimweleza Waziri (hayupo pichani) changamoto zinazowakabili juu ya Hifadhi ya mazingira.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment