MASIKINI ZOMBE...MWENZAKE CHRISTOPHER BAGENI AHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFU.. YEYE NA WENZAKE WAWLI.......


Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Ilala Christopher Bageni amehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya Mahakama ya Rufani Tanzania kutengua hukumu iliyomwachia huru na kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya wafanyabiashara wa madini watatu na dereva teksi mmoja.
Kadhalika mahakama hiyo imewaachia huru  Mkuu wa Upelelezi wa zamani (wakati huo Mkoa wa Dar es Salaam) (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi  mstaafu Abdallah Zombe na wenzake wawili baada ya ushahidi wa rufaa hiyo kushindwa kuwatia hatiani.

Mara baada ya hukumu kusomwa, ghafla Bageni aliduwaa wakati wenzake wakimkumbatia huku  wakibubujikwa na machozi wakiwa kizimbani. 
Wanaodaiwa kuwa wanafamilia wa washtakiwa hao waliangua vilio huku washtakiwa wenzake walisikika wakieleza masikitiko yao. Wengine walisikika wakisema angejua asingekuja mahakamani kusikiliza hukumu hiyo.
“Namshukuru Mungu...Lakini nasikitika kwa Bageni kukutwa na hatia sina raha kabisa....” alisema ASP Makele wakati akitoka katika ukumbi namba moja wa mahakama hiyo. 
Akizungumza baada ya hukumu hiyo,  ACP mstaafu Zombe alisema anamshukuru Mungu na kuhusu Bageni alisema hana cha kuzungumzia.
Hukumu hiyo imesomwa leo na Msajili wa mahakama hiyo Mhe. John Kahyoza baada ya rufani iliyokatwa na upande wa Jamhuri  kusikilizwa na jopo  la majaji watatu likiongozwa na Mwenyekiti, Jaji Bernard Luanda, Jaji Sauda Mjasiri na Jaji Semistocles Kaijage.
Msajili alisema awali Mahakama Kuu iliyoketi chini ya Jaji Salum Massati (wakati huo kabla ya kupanda kuwa jaji wa rufani), ilimuona Zombe na wenzake hawana hatia na kwamba haiwezi kuwahukumu kwa kosa la kusaidia kufanyika mauaji hayo.
Alisema Mahakama ya Rufani inakubaliana na Jaji Massati  kwamba mtuhumiwa hawezi kutiwa hatiani bila kuthibitisha mtu aliyetenda kosa hajashtakiwa na kutiwa hatiani.
“Jopo la majaji wa mahakama hii limeona ushahidi ulioeleza kwamba Bageni alikuwa eneo la tukio na kwamba alikuwa na mamlaka ya kuzuia mauaji yasitokee pamoja na kuwa hakuna ushahidi wa moja kwa moja kwamba aliona mauaji hayo yaliyofanywa na PC Saadi ambaye hajawahi kushtakiwa na siyo miongoni mwa washtakiwa waliotuhumiwa na mashtaka hayo.” Alisema wakati akichambua hukumu ya rufani hiyo.
Akifafanua zaidi hukumu hiyo alihoji, hakuna ubishi kwamba wafanyabiashara hao wakati wa uhai wao walipelekwa katika msitu wa Pande mahali ambako hakuna makazi ya watu wala nyumba kwa nini?  
“Katika ushahidi inasemekana kwamba Bageni kwa wadhifa aliokuwa nao, aliamrisha askari wa chini yake na gari kuelekea msitu wa Pande… Amri hiyo aliitoa kuelekeza gari hizo mahali ambako hakuna nyumba za kuishi bila sababu za msingi ili tukio ovu liweze kufanyika kwa kibali chake kama mkuu wa upelelezi” alisema msajili.
Hata hivyo, mashahidi wawili wa upande wa Jamhuri SP Mkumbi na SP Ubisimbali, pamoja na maelezo ya mshtakiwa Bageni, waliidanganya mahakama kwamba mauaji hayo yalifanyika eneo la Sinza baada ya majibishano kati ya polisi na wafanyabiashara hao wakati wa uhai wao, wakati wakijua mauaji hayo yalifanyika msitu wa Pande.
Msajili aliendela kusoma kwamba, maelezo na ushahidi wa mshtakiwa Koplo Rajabu amekiri kuwepo eneo la mauaji katika msitu wa Pande lakini hakushiriki mauaji hayo.
Hata hivyo, ushahidi huo wa utetezi ulipaswa kuwa wa Jamhuri na kuwepo na mwingine wa kuunga mkono lakini kuna ushahidi wa mawasiliano yaliyofanyika kati ya Zombe na Bageni kuhusu kutoa maelekezo ya mauaji hayo.
“Rufani hii inatengua kuachiwa huru Bageni na kumtia hatiani kwa mauaji na inampa adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
"Inawaachia huru mshtakiwa Zombe, Ahmed Makele na Koplo Rajabu...” alisema Msajili Kahyoza wakati akihitimisha hukumu hiyo.
Awali akichambua hukumu hiyo kuhusu Zombe na wenzake walioachiwa huru, msajili alisema ushahidi wa Koplo Rajabu haukuwa na nguvu ya kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa kuwa haukuungwa mkono na ushahidi wa Jamhuri.
Alisema kuhusu hoja za Jamhuri kuomba kuwashtaki Zombe na wenzake kwa kosa la kusaidia kuua hazina mashiko ya kisheria kwa sababu makosa hayo siyo yanayofanana dhidi ya washtakiwa - yaani mauaji na kusaidia kuua.
Alisema kila mshtakiwa anaposhtakiwa ana haki ya kujua shtaka analoshtakiwa nalo ili utetezi wake uelekeze dhidi ya mashtaka husika.

“Jaji ana mamlaka ya ya kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa ambalo hakushtakiwa nalo na aingie ndani kwa kina kwani bila kufanya hivyo itakuwa inamnyima haki mshtakiwa” alisema msajili.
Aprili 29, mwaka huu mahakama hiyo iliwaachia huru askari polisi watano kati ya tisa baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), kuona hana nia ya kuendelea na rufaa dhidi yao katika kesi ya mauaji ya watu wanne iliyokuwa na inawakabili pamoja na ACP Zombe. 
Aidha, mahakama iliwaachia baada ya DPP kuona kwamba rufaa hiyo haiwagusi askari hao kwamba hana nia ya kuendelea na rufani dhidi yao. 
Askari hao ni, Konstebo Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula, Koplo Michael Shonza, Koplo  Abineth Salo na Koplo Festus 
Gwabisabi. Hata hivyo, Dpp aliendelea na rufani  dhidi ya  ACP Zombe, SP Christopher Bageni, ASP Makelle na Koplo Bakari.
  
Mapema Mwaka 2006,  Zombe na wenzake walituhumiwa kufanya mauaji kwa makusudi dhidi ya wafanyabiashara watatu wa madini Sabinus Chigumbi maarufu kama Jongo, ndugu yake Ephrahim Chigumbi, Mathias Lunkombe na dereva teksi Juma Ndugu.

Ilidaiwa kuwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam, walalamikiwa waliwakamata watu hao wakiwa hai eneo la Sinza na kwenda kuwaua katika msitu huo. 

Oktoba 6, mwaka 2009 DPP alikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu hiyo kwamba Jaji Massati alikosea kuwaachia huru washtakiwa hao, kwa kuwa ushahidi wa Jamhuri ni dhahiri na wa mazingira unatosha kuwatia hatiani. 

Mei 8, mwaka 2013, Mahakama ilitupilia mbali rufaa hiyo kutokana na mapungufu ya kisheria.
Aidha, DPP alifungua maombi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, akiomba aruhusiwe
kukata tena rufaa hiyo nje ya muda ambayo yalikubaliwa.
Utetezi wa bageni;
Jaji: Mshitakiwa, hebu kwanza nikuulize, hii ripoti ya daktari hapa mimi bado inanisumbua kidogo, Kwanza umesema ulipokwenda katika ukuta wa Posta ulipopelekwa na James hamkukuta damu
Bageni: Ni kweli
Jaji: Jana yake siku mliyokwenda ama asubuhi yake kulikuwa na mvua?
Bageni: Hapana hapakuwa na mvua.
Jaji:Umesema ukutani uliona matundu sita yalidaiwa kuwa ni ya risasi, lakini hawa marehemu walikuwa ni wanne je hizi risasi sita zilitoka wapi au baada ya kupigwa waliendelea kupanda ukuta?
Bageni:Mtukufu Jaji. mimi sikuwepo lakini mapambano mengine  zinaweza kupigwa risasi nyingi zikajeruhi chache tu.
Jaji:Na kwa nini hapakuwa na damu?
Bageni: Mtukufu Jaji,hata mimi sijui kuwa ilikuwaje.
Jaji:Umesema matundu yale jinsi yalivyokuwa ukutani inaonekana yalipigwa kutokea pembeni, je katika hali hiyo inawezekanaje kumpiga mtu kisogoni?Alihoji Jaji na kumuelekeza Bageni aegemee ukuta na kisha kumtaka eleze mtu akipiga risasi kutokea upande wa kushoto kwake ni jinsi gani inaweza kumpata kisogoni.
Bageni: Mtukufu Jaji hapa zitampiga hapa,alisema Bageni akionyesha sehemu za begani.
Jaji:Umesema ulipelekewa maganda ya risasi baada ya siku tatu, nne je uliuliza kuwa maganda hayo waliyapata wapi?
Bageni: Niliuliza wakasema waliyatoa Sinza eneo la tukio.
Jaji:Waliya-collect siku hiyohiyo?
Bageni: Nadhani maana askari akipiga risasi lazima a-collect maganda.
Jaji:Kama pale ukutani kulikuwa na matundu sita na walikuletea maganda tisa je haya matatu uliuliza waliyatoa wapi?
Bageni: Ni kawaida Mtukufu Jaji kuwa unaweza kulenga risasi ikapita juu ya kitu ulichokusudia.
Jaji:Kwa maelezo ya James (mkuu wa upelelezi kituo cha Urafiki) ni askari wangapi waliopiga risasi siku hiyo?
Bageni: Hakunieleza ni wangapi.
Jaji:Balistic (Mtaalamu wa masuala ya silaha na milipuko) alisema ni silaha mbili tu ndizo zilizopia ya Saad na ya mshtakiwa wa 12 ,una ‘comment’ yoyote kwa hilo?
Bageni: Mtukufu Jaji, yeye ndiye mtaalamu.
Jaji:Umeeleza kuwa mshtakiwa wa kwanza alikushauri lini mbadili taarifa ya kwenda kwenye Tume ya Kipenka?
Bageni: Mtukufu Jaji, sikuwa specific katika tarehe ila rekodi isomeke siku ambayo alikuwa ‘summoned’ kwenye tume.
Jaji:Kwa nini alikwambia uandike nyingine wakati ulikwishaandika taarifa ya kwako?
Bageni:Aliniambai ifanyiwe marekebisho kidogo ili mambo yawe sawa.
Jaji:Mshtakiwa wa kwanza alisema hapa kuwa polisi hutii amri halali tu je hiyo ilikuwa ni amri halali?


Bageni:Ni halali sababu yeye ni mkubwa wangu
  
Agosti 17  mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, iliyoketi chini ya Jaji Massati ilitoa hukumu iliyomwachia huru Zombe na wenzake, baada ya ushahi wa upande wa  jamhuri kushindwa kuwatia hatinai.
Baada ya hukumu hiyo ya mahakama kuu, DPP (wakati huo Eliezer Feleshi) hakulidhishwa na hukumu hiyo Oktoba 7, mwaka 2009 alikata rufani Mahakama ya Rufani ,  kupinga hukumu hiyo.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment