MAKAMU WA RAIS MHE. SAMIA AFUNGUA KONGAMANO LA PILI NA MAONESHO YA KITENGO CHA WAHANDISI WANAWAKE CHA TAASISI YA WAANDISI TANZANIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan aonyesha zawadi ya Saa aliopewa na Wahandishi Wanawake (TAWESE) kwenye Kongamano la Pili la Maonesho ya Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Waandisi Tanzania.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akizungumza na Mhandisi Mshauri Bi. Warda Ester Mash'mark alipotembelea banda lake wakati wa Kongamano la Pili la Maonesho ya Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Waandisi Tanzania.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi Anifa chingumbe wa TTCL namna ambavyo mtandao wa 4G LTE unavyofanyakazi alipotembelea banda la TTCL kwenye Kongamano la Pili la Maonesho ya Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Waandisi Tanzania.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  Hassan akihutubia kwenye Kongamano la Pili la Maonesho ya Kitengo cha Wahandisi Wanawake cha Taasisi ya Waandisi Tanzania.
Sehemu ya Waandishi waliohudhuria Kongamano hilo wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Rais.
Msajili wa Bodi ya Wahandisi, Mhandisi Steven Mlote akihutubia kwenye Kongamano hilo la Wahandisi Wanawake.
Mwakilishi wa Balozi wa Norway akihutubia kwenye Kongamano hilo la Wahandisi Wanawake lililofanyika kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.
 
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka wahandisi wanawake nchini kufanya kampeni maalum ya kushawishi watoto wa kike kujenga ari ya kusoma masomo ya sayansi na hisabati kama hatua ya kuongeza maradufu wahandisi wanawake nchini.

Makamu Rais ametoa kauli hiyo 12-Aug-16 wakati anafungua kongamano la maonyesho ya kitengo cha wahandisi wanawake cha Taasisi ya Wahandisi Tanzania katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa kampeni hiyo itasaidia kuelimisha wasichana,kuwaunganisha na kuwaendeleza watoto wa kike ili waweze kujitambua na kuithamini nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya nchi kupitia fani za sayansi na teknolojia.

Makamu wa Rais amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa wahandisi katika maendeleo ya nchi hususani katika sekta za nishati,madini,barabara,maji,uvuvi na kilimo imeendelea kuweka mipango madhubuti ya kuinua na kuimarisha fani ya uhandisi hapa nchini.


Ameeleza kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ya kuongeza vyuo vya uhandisi kutoka chuo Kimoja mwaka 1970 mpaka vyuo Tisa hivi sasa na kuongeza maabara katika shule za umma ili kuwavutia wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan pia amepongeza baadhi ya halmashauri nchi ambazo zimekamilisha ujenzi wa maabara kwenye shule za sekondari na kuweka vifaa vyote vya kujifunzia.

Kuhusu wakandarasi wa ndani ya nchi, Makamu wa Rais amesema serikali itaendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa wenye uwezo katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa barabara ili kuwajengea uwezo.

Amesisitiza kuwa matumizi ya wakandarasi wazawa wenye uwezo wa kufanya kazi yatasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza ajira kwa vijana wa kitanzania kuliko kutumia wakandarasi wa nje ambao mara nyingi baadhi yao wanaajiri watalaamu kutoka kwenye nchi wanazotoka kuliko kuajiri Wataalamu wa hapa nchini.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameshauri Taasisi ya Wahandisi Tanzania iendelee na jukumu la kuwaunganisha wahandisi wote watanzania ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya taifa na ameishukuru serikali ya Norway kwa mchango wao wa shilingi bilioni 4.3 ili kuchangia mpango wa miaka Mitano kuanzia mwaka 2016 hadi 2021 ambao utasaidia kuwajengea uzoefu wahandisi wanawake ili waweze kusajiliwa na bodi ya usajili ya wahandisi nchini.

Makamu wa Rais amesema mpango huo pia unatarajiwa kunufaisha wanafunzi wa kike 150 nchini na utaisaidia serikali kufanikisha lengo la kufikia uchumi wa viwanda na kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi,Teknolojia na Ufundi Mhandisi Stella Manyanya ameiomba serikali ihakikishe inakamilisha mpango wa kuweka vifaa kwenye maabara za shule za sekondari kote nchini kama hatua ya kuwavutia wasichana wengi kusoma masomo ya sayansi.

Kulingana na takwimu za Kitengo cha Taasisi ya Wahandisi Wanawake Tanzania idadi ya wahandisi wanawake imeongezeka kutoka wanawake 35 mwaka 2005 hadi wanawake wahandisi 298 mwaka 2015.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment