MAANDALIZI YA UKUTA SEMPTEMBAR MOSI YAIVA HAYA PAMA NDIO MAAMUZI YAKIYOVIKIWA LEO


TAARIFA KWA UMMA

TAMKO LA VYAMA VYA SIASA VYA ACT-WAZALENDO, CHADEMA, CUF, NA NCCR-MAGEUZI, KUTOKANA NA KIKAO CHA VIONGOZI WA DINI NA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA VYENYE UWAKILISHI BUNGENI: 

Imetolewa leo tarehe 25/8/2016

Kutokana na kikao kilichofanyika jana tarehe 24/8/2016 kati ya viongozi wa dini na vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni juu ya hali ya mahusiano na ushiriki wa wabunge katika vikao vya bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na athari zake kwa wananchi, pia kikao hicho kilijadili mvutano kati ya CHADEMA na vyombo vya dola kuhusiana na maandalizi ya Operesheni UKUTA yanayoendelea nchini na suala la hali ya kisiasa Zanzibar. Kikao hicho kilifanyika katika Hotel ya Courtyard iliyopo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini hapa nchini pamoja na waziri wa mambo ya ndani ya nchi Ndugu Mwigulu Nchemba, kwa uratibu wa CCT, BAKWATA NA TEC.
Vyama vya siasa vya ACT-WAZALENDO, CHADEMA, CUF, NA NCCR-MAGEUZI, Vinapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza viongozi wa dini kwa jitihada zao za kuwakutanisha viongozi wa kisiasa na serikali kuzungumzia mustakbali wa hali ya kisiasa nchini hususani juu ya ukandamizwaji wa demokrasia na ukiukwaji wa haki za binaadamu, uhuru na haki za kikatiba kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake aidha, ulijadiliana juu ya vitisho vya vyombo vya dola dhidi ya vyama vya siasa, wananchi na kutolewa kwa kauli zinazopingana na katiba na sheria za nchi yetu.
Kutokana na mwenendo usiofaa wa Naibu spika wa Bunge Tulia Ackson tumepokea na kukubaliana kwa pamoja kuwa viongozi wa vyama vya upinzani vyenye wabunge watakaa na kujadili na kuona ni jinsi gani suala hili linapatiwa ufumbuzi kama mheshimiwa Spika Job Ndugai alivyoshauri kwenda katika majadiliano ili kupata maridhiano. 
WITO WETU KWA VIONGOZI WA DINI, SERIKALI INAYOONGOZWA NA CHAMA CHA MAPINDUZI NA WATANZANIA KWA UJUMLA;
VIONGOZI WA DINI:
1. Kwa pamoja vyama vyetu vinawaomba viongozi wa dini kuendelea na jitihada hizi bila kuchoka za kuwaleta watanzania wote pamoja na kuhakikisha HAKI, AMANI, MSHIKAMANO, NA UMOJA WA KITAIFA UNADUMISHWA kwa kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinafuata na kuheshimiwa kikamilifu na mamlaka zote za nchi na viongozi wote wa kisiasa. Viongozi wa dini wajitahidi kadri inavyowezekana kutojifungamanisha na upande unaokandamiza HAKI, KATIBA, SHERIA, TARATIBU NA KANUNI ZA UENDESHAJI WA NCHI YETU. 

2. Kwa pamoja vyama vyetu vinawaomba viongozi wa dini kuwafikia viongozi wenye mamlaka ya uendeleshaji wa serikali, vyombo vyake (Jeshi la polisi) na taasisi mbalimbali akiwemo Mheshimiwa Rais na kumnasihi na kumuelezea juu ya umuhimu wa kila mtanzania kuheshimu na kufuata sheria za nchi yetu na taratibu zake bila kuivunja katiba ya nchi ambayo watendaji wakuu wote wa serikali waliapa kuilinda na kuihifadhi, kwa namna yeyote ile na kwa visingizio vyovyote vile hawapaswi kukiuka kiapo hiki.
3. Kwa pamoja vyama hivi vimekubaliana na kuwaomba viongozi wa dini kuingilia kati hali ya kisiasa inayoendelea visiwani Zanzibar kufuatia kufutwa kwa maamuzi halali ya wananchi waliyoyafanya kupitia uchaguzi mkuu wa tarehe 25 Oktoba, 2015. Viongozi wa dini wanapaswa kuingilia kati kwa lengo la kurejesha demokrasia, haki za binadamu, utengamano wa kitaifa, amani, utulivu na kuwaondolea hofu wananchi dhidi ya vitisho vya vyombo vya dola. Na kwa vyovote vile ili kuleta umoja wa kitaifa, kudumisha amani na utulivu na maendeleo endelevu ya kiuchumi na kisiasa nchini serikali ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ) hazina budi kuamini katika misingi ya maridhiano, utawala wa sheria, na uhuru wa kidemokrasia.

WITO KWA VIONGOZI SERIKALI INAYOONGOZWA NA CCM:

4. Vyama vya siasa vya ACT-WAZALENDO, CHADEMA, CUF, NA NCCR-MAGEUZI, vinasikitishwa na namna serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli kukosa uvumilivu wa kisiasa na badala yake kuendesha nchi kwa mfumo wa mabavu bila kuzingatia sheria, haki na wajibu, taratibu na kanuni tulizojiwekea za uendeshaji wa nchi yetu.

5. Kwa pamoja tunamtaka Rais magufuli asione aibu kuiga busara za aliyekuwa spika wa bunge lililopita mama Anna Makinda pale kila palipotokea sintofahamu baina yetu hakusita kutupeleka katika meza ya maridhiano na kulipatia ufumbuzi kwa njia za busara na hekima hata pale suala hilo lilikuwa linamgusa yeye mwenyewe.

6. Kwa pamoja hatukubaliani na maamuzi ya serikali yake kuliweka bunge gizani, kufanya matumizi ya fedha za umma bila kuzingatia bajeti iliyopitishwa na Bunge, kuzuia vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria, kuzuia mikutano ya hadhara, kuzuia vikao vya ndani vya vyama vya siasa, kuzuia makongamano ya kujadili mustakbali wa Taifa letu kama ambavyo chama cha ACT-Wazalendo kulivyozuliwa kufanya kongamano la kujadili bajeti ya serikali 2016/17, Rais Magufuli asijifiche katika kichaka cha dola, ajitokeze hadharani kama anaona hawezi kuongoza nchi katika mfumo wa vyama vingi ulioridhiwa kikatiba, tunamshauri aiagize serikali yake iwasilishe muswada wa dharura katika bunge lijalo ili kufuta vyama vyote vya siasa na aendeleshe nchi kwa namna anayoitaka yeye binafsi. Tunamtaka Rais Magufuli atambue kuwa kamwe hatoweza kuzuia nguvu ya umma iliyo tayari kuleta mabadiliko sahihi ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, na kuboresha hali za maisha na kipato cha mtanzania kwa kutumia vyema rasilimali za nchi yetu.  

7. Kwa pamoja tunatambua kuwa, ili Taifa letu liwe salama ni lazima tumzuie Rais kwa njia ya amani asiendelee kuikanyaga katiba ya nchi aliyoapa kuilinda kwa kutoingilia utendaji wa mihimili mingine. Tunahitaji Taifa letu liwe salama na hatuhitaji kwa namna yeyote ile uvunjwaji wa sheria na matumizi ya nguvu kubwa za vyombo vya dola yanayoandaliwa kwa madhumuni ya kuwajengea hofu watanzania na umwagaji wa damu unaopangwa kufanywa na vyombo hivyo.  
WITO KWA WATANZANIA WOTE:
8. Vyama vya Siasa vya ACT-WAZALENDO, CHADEMA, CUF, NA NCCR-MAGEUZI, vinawataka watanzania wote bila ya kujali itikadi za vyama vyao kusimama imara kutetea misingi ya uongozi wa Taifa letu kwa kuilinda na kuihifadhi katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuhakikisha inaheshimiwa, inafuatwa na kuhuifadhiwa na kila mmoja wetu.

9. Kwa pamoja Tunapenda kuwafahamisha watanzania kuwa serikali ya awamu ya tano imejawa na hofu ya nguvu ya mabadiliko inayotokana na wananchi na sasa imeamua kutumia vitisho kwa kuliamuru jeshi la Polisi kufanya mazoezi ya kijeshi hadharani na kutumia silaha nzito, lengo likiwa ni kutaka kuwaogopesha juu ya kusimamia haki yenu ya kidemokrasia. 

10. Tunawasihi muendelee kutuunga mkono pale tunaposimama kwa niaba  yenu kuhakikisha haki hii ya upatikanaji wa uhuru wa demokrasia inalindwa kwa kuwa ni wazi tutakabiliana na madhila kadhaa kutoka kwa waliodhamiria kuisigina katiba ya nchi kwa kutumia dhamana walizowakabidhi.

Kwa pamoja ACT-WAZALENDO, CHADEMA, CUF, NA NCCR-MAGEUZI, tunawahakikishia watanzania wote kuwa vyama vyetu vitaendelea kuimarisha umoja na mashirikiano baina yetu ya KUDAI HAKI SAWA KWA WOTE, DEMOKRASIA YA KWELI, MAGEUZI NA UZALENDO WA KWELI NA DHATI kwa maslahi mapana ya Taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Hatutarudi nyuma kudai haki zetu za kikatiba na kisheria Tutaunganisha NGUVU ZA UMMA NA NGUVU YA MABADILIKO ili 

kuwawezesha watanzania kuipata Tanzania waitakayo
 kwa kutumia njia za amani na kidemokrasia.

JAMES FRANCIS MBATIA               _____________________________
MWENYEKITI TAIFA NCCR-MAGEUZI

SAID ISSA MOHAMED                  ______________________________
MAKAMU MWENYEKITI TAIFA 
CHADEMA ZANZIBAR

SHAWEJI M.MKETO           _____________________________
NAIBU MKURUGENZI WA OGANAIZESHENI 
NA UCHAGUZI CUF TAIFA

ADO SHAIBU                                  _____________________________
KATIBU WA ITIKADI, MAWASILIANO NA UENEZI TAIFA 
ACT- WAZALENDO

Maharagande Mbarala
Mratibu 0784 001 408
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment