DC HAPI AWABAINI WANAFUNZI HEWA KINONDONI WANAOPATA FEDHA ZA ELIMU BURE

DC HAPI AWABAINI WANAFUNZI HEWA KINONDONI WANAOPATA FEDHA ZA ELIMU BURE
*NI KUFUATIA AGIZO LA RAIS MAGUFULI 

*WAKUU WA SHULE 68 MSINGI NA 22 SEKONDARI KUSHUSHWA VYEO, KUCHUKULIWA HATUA KALI 

Wakati serikali ya awamu ya Tano ambayo inaongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ikiahidi elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka sekondari ambapo serikali inatumia shilingi Bilioni 18 kila mwezi, wilaya ya Kinondoni imefanya uchunguzi wa kina na kubaini udanganyifu mkubwa uliofanywa na wakuu wa shule 68 za msingi na 22 za sekondari wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mh. Ally Hapi amesema aliagiza uchunguzi huo kutekeleza agizo la Rais John Magufuli alilotoa kwa wakuu wa wilaya kuwachukulia hatua kali walimu wakuu na watendaji wote ambao watafanya udanganyifu na ubadhirifu wa fedha za elimu bure.

Hapi amebainisha leo ofisini kwake mbele ya waandishi wa habari kuwa wanafunzi 3,462 wa shule za msingi na 2,534 wa sekondari wemebainika kuwa ni hewa na fedha zao hazikupaswa kupelekwa.

"Baada ya agizo la Mh. Rais kule Shinyanga, na maagizo mengine ya kusimamia elimu bure ambayo amekua akiyatoa kwetu sisi wasaidizi wake katika vipindi tofauti, tuliamua kufanya uhakiki wa wanafunzi wetu darasa kwa darasa. Lengo lilikua ni kujiridhisha kama taarifa ambazo tunapewa na wakuu wa shule ni sahihi au ni za uongo. Tumebaini udanganyifu mkubwa na tayari nimeagiza Mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni awavue madaraka walimu wakuu 68 wa msingi ambao wako kwenye mamlaka yake na kisha kuwafikisha kwenye tume ya utumishi wa walimu na vyombo vingine vya kisheria kwa hatua zaidi. Badala yake vyeo hivyo nimeelekeza wapewe vijana, wenye sifa, waaminifu kwa taifa, Wazalendo na wachapakazi."

Aidha kuhusu walimu wakuu wa shule za sekondari waliobainika kufanya udanganyifu na ubadhirifu wa ruzuku ya elimu bure, Mh. Hapi amesema..

"Hawa wakuu wa shule 22 za sekondari mamlaka yao ni katibu tawala wa Mkoa. Tayari tumemuandikia barua Katibu tawala wa Mkoa ili awachukulie hatua ikiwemo kuwavua madaraka yao na kuwapa walimu wengine waadilifu, Wazalendo na wachapakazi. Katika wilaya yangu sitaki kuwaona wakiendelea kuwa wakuu wa shule tena. Natoa rai kwa watendaji wengine wa Kinondoni wasio waaminifu na Wazalendo na wasiofuata sheria na taratibu, kuwa popote walipo tutawasaka na watakwenda na maji wasipojirekebisha na kuendana na kasi ya Rais wetu Dr. John Magufuli."

Mwishoni mwa mwezi Julai, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Magufuli alitoa maagizo kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi nchini kufuatilia kwa makini fedha za elimu bure ili kubaini udanganyifu na wizi unaofanywa na watendaji wasio waadilifu. Rais Magufuli aliyasema hayo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga.
Kinondoni inakua ni wilaya ya kwanza kutekeleza agizo la Mh. Rais katika kipindi cha wiko mbili tu tangu agizo hilo kutolewa.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment