TRA Yaifungia Kampuni ya Mkono kwa Kudaiwa kodi Sh. Bilioni 1.1


Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupitia kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart & Co imeifungia kampuni ya Mkono & Company Advocate kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya kodi inayofikia Sh1 bilioni.

Kampuni hiyo inahusishwa na Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono (CCM) ambaye pia ni wakili maarufu nchini.

Hata hivyo, Mkono hakupatikana mara moja kuzungumzia suala hilo. Hati ya TRA iliyosainiwa na Kamishna wa TRA, Neema Mrema imesema Yono imepewa mamlaka na Kamishina Mkuu wa mamlaka hiyo chini ya kifungu cha 64 cha Sheria ya Kodi ya mwaka 2015 ya kushika mali za mdaiwa anayeshindwa kulipa kodi.

“Naomba kupata usaidizi wa Yono Auction Mart & Company Ltd na Polisi kutaifisha na kuhamisha bidhaa na mali popote zilipo ili kwa njia yoyote zikiuzwa zilipe deni jumla ya Sh1,101,432,045.99 pamoja na gharama za wito uliotolewa chini ya Kamishna….” ilisema sehemu ya hati hiyo.

Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa Yono Auction Mart Co. Ltd, Stanley Yono alikiri kuifungia kampuni hiyo mpaka itakapolipa deni hilo.

“Ni kweli tumeifungia kampuni ya uwakili ya Mkono na hapa tuko kwenye eneo la tukio. Anadaiwa zaidi ya Sh1 bilioni ikiwa ni malimbikizo ya VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani), kodi za mishahara na nyinginezo kwa mwaka mzima. Amegoma kutia saini hii hati lakini haitasaidia kitu kwani tumeshamfungia,” alisema Yono.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Mlipa kodi wa TRA, Richard Kayombo alikiri kuifungia kampuni hiyo.

SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment