TAARIFA KWA UMMA KUTOKA MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA.


WIZARA YA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA

TAARIFA KWA UMMA

MAELEKEZO JUU YA MIRADI YA UBUNIFU WA KUTENGENEZA NDEGE

1.         UTANGULIZI

1.1.    Taarifa hii kwa umma imetolewa kwa mujibu wa madaraka ya kisheria aliyonayo Mkurugenzi Mkuu kupitia sheria ya Usafiri wa Anga nchini, sheria namba 80 (iliyofanyiwa maboresho mwaka 2006) pamoja na kanuni zake mbalimbali zilizopo zikiwa na lengo la kuhakikisha hususan usalama katika usafiri wa anga pamoja na kulinda maslahi ya wananchi na mali zao kwa ujumla kutokana na shughuli za usafiri wa anga.

 1.2.    Taarifa hii kwa umma imetolewa ili kuufahamisha umma kwa ujumla juu ya tahadhari za ki-usalama za kuzingatiwa pindi unapofanya shughuli za uendeshaji wa usafiri wa anga nchini Tanzania. Taarifa hii kwa umma imetolewa kufuatia Mamlaka kubaini kwamba hivi karibuni kumeibuka wimbi la watu binafsi pamoja na taasisi zinazodai kuwa na uwezo wa kutengeneza ndege(Helikopta) na wapo katika hatua ya kuzifanyia majaribio ya kuzirusha angani pasipo kuzingatia  kanuni za usafiri wa anga na taratibu zake za ki- usalama zilizopo.


1.3.    Taasisi ama mtu yeyote anayetarajia kutengeneza ndege au vifaa vyake   anakumbushwa kuhakikisha anafanya hivyo kwa mujibu wa kanuni za usafiri wa anga ikiwemo pamoja na kupata kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania kabla ya kuanza mradi wake.

1.4.    Lengo ni kuhakikisha usalama kwa wananchi na mali zao, kuzingatia viwango vya ubunifu husika, aina na ubora wa  malighafi   zinazotumika kufanya ubunifu, vipuri vya ubunifu husika,  jinsi ya uundwaji wa  chombo husika unavyofanyika  hasa kuangalia kama vifaa vinavyotumika kutengenezea ndege ni vile vinavyokubaliwa na kanuni za Mamlaka ya usafiri wa anga nchini  pamoja na zile za kimataifa .

2.    KUTAMBULIWA KWA NDEGE  

2.1.    Kanuni namba 5 ya usafiri wa anga (inayohusu ubora wa ndege) kanuni ya mwaka 2011 imeweka  bayana kwamba:
2.1.1     Mamlaka italitambua ombi ama wazo la kutaka kutengeneza ndege, vifaa vya ndege  endapo Mamlaka itajiridhisha kwamba,

(a)  Kazi itakayofanywa ni ile inayoendana na miundo inayokubaliwa katika utengenezaji wa ndege;
(b)  Uwepo wa utaratibu maalum ikiwa ni pamoja na uwepo wa usimamizi wa mhandisi mwenye cheti cha kutengeneza  aina ya ndege husika atakayehakikisha anasimamia hatua zote za ubunifu na ufundi wa ndege husika ; na
(c)  Taratibu za maandalizi yake zinakubaliwa katika kutengeneza ndege husika.


3.      UBUNIFU NA MATENGENEZO YA NDEGE
3.1 Kanuni za kimataifa kama zilivyoainishwa na ICAO kwenye Annex namba 8 (inayohusu ubora wa ndege) zimeanisha kwamba “Maelezo ya kubuni na kuunda ndege lazima yaweze kuthibitibisha bila ya shaka kwamba vipuri vyote vya helikopta husika vitafanya kazi kwa uhakika na kwa usalama katika mazingira mbalimbali iwapo angani. Na lazima iwe imetokana na tafiti za kina zilizofanywa na kuthibishwa kutoa majibu ya kuridhisha au iwe imethibitishwa kwa majaribio maalum au kwa kupitia tafiti maalum za watafiti waliobobea katika masuala ya anga au iwe imepitia hatua zote hizo kwa ujumla.

3.2 Tanzania kwa sasa haina wataalamu waliobobea katika kudhibiti shughuli za utengenezaji ndege, wala kuwa na taasisi ama viwanda vinavyotengeneza  ndege wala viwanda vya vipuri vya ndege ili kuweza kuthibisha ubora na ufanisi wa vifaa hivyo. Hata hivyo Mamlaka inaweza kuandaa utaratibu kwa kupitia washirika wake na Mamlaka zingine za usafiri wa anga duniani (mfano Mamlaka ya usalama wa Anga ya Ulaya (EASA) au Idara ya usalama wa Anga ya Marekani (FAA) ili kuweza kusaidia kuhakikisha kwamba kabla bidhaa husika haijaanza kutumiwa na umma, hatua zote za ubunifu, malighafi zake ziwe zimefanyiwa majaribio stahiki ili kuweza kuhakikisha kwamba bidhaa husika inaweza kuhimili mazingira magumu ya hewa iwapo angani bila kuleta athari. Hatua zote ikihusisha injini, mota na mabawa ya ndege  husika nk yawe yamekidhi na kufaulu majaribio mbali mbali ya kuhimili mazingira magumu ya hewa angani.


4.      HITIMISHO

4.1 Ili kuendelea kulinda usalama kwa umma, taasisi ama mtu binafsi anapaswa kuhakikisha anazingatia sheria za usafiri wa anga pamoja na kanuni zake. Kuanzia sasa si ruhusa kwa yeyote kujihusisha na ubunifu wa ndege, kutengeneza ndege ama vifaa vya ndege  bila kuwasiliana na Mamlaka ili kuweza kupatiwa maelekezo na hatua stahiki zinazopaswa kupitia na kuzingatia ili hicho kinachondaliwa kiwe kimezingatia taratibu za kimataifa za utengenezaji ndege.

4.2  Mamlaka inaunga mkono ubunifu wa aina hii katika masuala ya usafiri wa Anga, ila inapaswa kufanywa kwa mujibu wa taratibu maalum ili kuhakikisha usalama. Sambamba na hili wataalamu wa masuala ya usafiri wa anga wa Mamlaka watawatembelea wabunifu  husika waliojitokeza ili kuweza kuwapatia ushauri na  maelekezo zaidi.

4.3 Kwa kutolewa kwa taarifa hii, tunatoa wito kwa watu binafsi ama taasisi kusitisha shughuli zote za utengenezaji wa ndege na wanaombwa kuwasiliana na Mamlaka ya usafiri wa anga kwa maelekezo na miongozo zaidi kwa mujibu wa sheria.


Imetolewa na
Hamza S. Johari
MKURUGENZI MKUU
 MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA

JULAI  2016
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment