KIJANA GOZBERT BWELE ALIVYOMPAGAWISHA MAKAMU WA RAIS WA HISPANIA MJINI NANSIO

WAKATI wasanii wa kundi la ngoma za utamaduni la Utandawazi wanajipanga kutumbuiza, watu wengi waliokusanyika kwenye viwanja wa shule ya msingi Bukongo mjini Nansio walikuwa wanajiuliza mtoto Gozbert Bwele (8) aliyekuwa amekumbatia ngoma alikwenda kufanya nini pale.
Lakini mara tu ngoma zilipoanza kupigwa, uwanja mzima ukalipuka kwa furaha na haikushangaza wakati makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, Mama Maria Teresa Fernandez de la Vega, aliposhindwa kuvumilia na kutoka kwenda kucheza na mtoto huyo aliyeonyesha ufundi mkubwa katika upigaji wa ngoma.
Mama Maria Teresa, ambaye ni rais wa taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, alijitoma uwanjani kucheza na kumtunza mtoto huyo anayesoma darasa la kwanza kwenye shule ya msingi Nansole katika halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.
Makamu huyo wa rais mstaafu wa Hispania alizuru kisiwani Ukerewe akiwa ameongozana na ujumbe wake kwa lengo la kujionea kilimo cha viazi lishe na usindikaji wa mazao mbalimbali yatokanayo na viazi hivyo.
Kilimo hicho kinafanywa na akinamama 25 chini ya Mradi wa Green Voices unaofadhiliwa na taasisi ya Mfuko wa kusaidia Wanawake Afrika, ambao kwa hapa nchini  umewawezesha wanawake wa Tanzania kubuni miradi endelevu inayoendana na utunzaji wa mazingira pamoja na kupambana na mabadiliko ya tabianchi.
Mtoto Gozbert Bwele akiwajibika na ngoma yake.

Gozbert Bwele siyo tu alionekana kukibeba kikundi hicho na kuwafanya wananchi waliokusanyika kumtupia macho yeye na kusahau kama kulikuwa na wasanii wengine, bali alionyesha uhodari mkubwa wa kupiga ngoma kwa mbwembwe nyingi huku akitumia kichwa, miguu na makalio, akilala na ngoma bila kupoteza midundo ya ngoma na wimbo.
Noti nyekundu zilikuwa zikipepea usoni kama maua, lakini hakujisumbua kupokea wala kuokota hata moja, bali ndiyo kwanza akaongeza ufundi katika kukung’uta ngoma huku akiimba.
“Ninapenda sana kupiga ngoma,” ndivyo anavyosema Gozbert ambaye anabainisha kwamba katika familia yake hakuna msanii isipokuwa yeye pekee.
Anaongeza: “Tangu utotoni nilipenda kupiga ngoma, nilikuwa natumia vikopo, lakini nikaona havinitoshi.”
Kebela Mganga ni kiongozi wa kikundi cha Utandawazi Theatre Matwi ga charo (Masikio ya Dunia), ambaye anaeleza historia ya mtoto Gozbert, ambapo anasema mtoto huyo aliibuka tu kwenye mazoezi ya kikundi chao.
“Miaka sita iliyopita, yaani mwaka 2010, tulishangaa kuona mtoto mwenye miaka kama miwili hivi akiingia kwenye mazoezi yetu na kusema anataka kujifunza kupiga ngoma, yeye alitaka ngoma tu,” anasema Kebela.
Anaongeza: “Wakati huo tulikuwa tunajiandaa kwenda Bagamoyo, hivyo tukamwambia kwamba asubiri kwanza turudi. Kwa hiyo mwaka uliofuata akiwa na miaka mitatu tu akajiunga nasi na tukaenda naye Bagamoyo pale Chuo cha Sanaa.”
Mpaka sasa ameshashiriki matamasha mbalimbali ndani na nje ya nchi ambapo Desemba 9, 2012 alishiriki sherehe za uhuru jijini Dar es Salaam.
Wasanii wa kundi la Utandawazi Theatre ‘Matwi ga charo’ la Nansio, Ukerewe, wakitumbuiza wakati wa ziara ya makamu wa rais mstaafu wa Hispania, Maria Teresa Fernandez de la Vega (hayupo pichani) katika viwanja vya shule ya msingi Bukongo mjini Nansio.

“Mwaka 2013 tulikwenda naye kwenye sherehe za uhuru wa Rwanda na kule aliacha gumzo kubwa, mwaka 2014 tulikwenda naye kwenye Sherehe za Mapinduzi Zanzibar na mwaka 2015 tulikwenda naye kwenye Maonyesho ya Kilimo Zambia, ni msanii mahiri sana na tegemeo kwetu,” anasema Kebela.
Kebela anasema kwamba, katika kundi lao yupo pia binti wa miaka 8 pia ambaye ni mahiri katika uchezaji wa ngoma.
Anaeleza kwamba, wanawalea watoto hao kama wa kwao, lakini shule ndiyo kitu cha kwanza kuwahimiza ili waweze kuwa na msingi mzuri.
“Wote wanajitahidi sana shule, na tunawahimiza wazingatie masomo,” anasema na kuongeza kwamba wanapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wazazi wa watoto hao.

Mama Maria Teresa anapenda sana watoto. Hapa aliamua kusitisha ziara kwa muda baada ya kumkuta mtoto huyu akiwa na mama yake wakiwa nje ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment