Amchapa fimbo mkewe, amuua


WAKAZI wawili wa wilaya ya Tarime, mkoani Mara wameuawa katika matukio mawili tofauti, likiwemo la mwanamke kuuawa na mume wake kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili.

Kamanda wa polisi wa Tarime-Rorya, Andrew Satta alisema mkazi wa Nyangoto, Nyamongo Magaigwa (28) aliuawa kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali mwilini na mume wake Hamis Mtundi(37).

Katika tukio lingine, Kamanda Satta alisema Charles Juma aliuawa kwa kupigwa kwa fimbo kichwani na ubavuni na Chacha Msabi wakati wakiwa katika Baa ya Siwa iliyopo Sirari mpakani.

Kamanda Satta alisema katika tukio la kwanza lililotokea Juni 30, mwaka huu katika Kitongoji cha Stooni, kijiji cha Nyangoto- Nyamongo ulitokea ugomvi unaotokana na wivu wa mapenzi kati ya Mtundi na mke wake Nyamongo aliyerudi nyumbani akiwa amelewa.

Alisema mtuhumiwa alimshambulia mkewe kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili ambaye alifariki njiani wakati akikimbizwa katika hospitali ya wilaya kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Mtuhumiwa huyo anashikiliwa kwa mahojiano zaidi na kisha atafikishwa mahakamani. Katika tukio la pili lililotokea Juni 27, mwaka huu katika Kitongoji cha Forodhani Sirari kwenye baa ya Siwa, ulitokea ugomvi kati ya Chacha Msabi na Charles Juma.

Alisema Msabi alimpiga Juma kichwani na ubavuni kwa kutumia fimbo aliyokuwa nayo na kusababisha majeraha makubwa kichwani na maumivu makali na kukimbizwa katika hospitali ya wilaya kupatiwa matibabu na ilipofika Juni 28, majeruhi huyo alifariki dunia.

Mtuhumiwa baada ya tukio hilo alitoroka na anatafutwa na polisi. Aliomba wananchi kutoa taarifa watakapomuona Msabi ili aweze kukamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kujibu mashitaka yanayomkabili.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment