Waziri Nape Nnauye akutana na Wanachama wa Shirikisho la kazi za Sanaa za Ufundi Tanzania.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (kushoto) akipokea maelezo kuhusu sanamu iliyochongwa toka kwa Mwandamizi na Msemaji wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) Bw. Nyunga Joseph Nyunga wakati alipotembela katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (wa tatu kushoto) akiangalia kazi za sanaa ya uchongaji ndani ya moja ya mabadanda ya Wachongaji hao wakati alipotembela katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye (katikati) akiwa ameongozana na baadhi ya Viongozi wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) wakati alipowasili katika eneo lao lililoko Mwenge, jijini Dar es Salaam, 28 Juni, 2016.PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM.


Na Benedict Liwenga-WHUSM.

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ameahidi kuzitataua baadhi ya changamoto mbalimbali zinazoikabili Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) ikiwemo upatikanaji wa Hati Miliki ya Kiwanja kwa ajili ya kazi zao, Ushuru unaotozwa kupitia Idara ya Maliasili nchini pamoja na Sheria ya Tozo katika Viwanja vya Ndege.

Mhe, Nnuaye ametoa ahadi hiyo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na Wanachama wa Shirikisho hilo ambapo amesema kuwa, suala la upatikanaji wa Hati Miliki ya eneo kwa ajili ya kazi za Wachongaji hao alishaanza kuifanyia kazi kwa kufanya mawasiliano na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi na amewahakikishia kwamba Hati ya eneo hilo itapatikana ili Wachongaji hao waweze kuwa na eneo lao maalum la kazi zao.

‘’Suala la upatikanaji wa Hati Miliki katika eneo lenu ambalo limekuwa likileta minong’ono niachieni mimi kwani najua katika hili kuna baadhi ya watu wenye fedha wanataka kuwakandamiza watu wasio na uwezo kwa kudai kuwa eneo ni la kwao, hapo awali nilishafanya mazungumzo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na nawahahakikishieni kuwa haki itatendeka, kwani hakuna mtu mwenye mfuko mkubwa wa kuweza kuiingiza Serikali nzima katika suala hili’’, alisema, Mhe. Nnauye.

Kuhusu suala la Ushuru unaotozwa na Maliasili nchini, Mhe. Nnauye amesema kuwa yuko tayari kukaa na watu wa Maliasili na kuona namna gani ushuru huo unavyotozwa hususani kwa Wachonagji hao pasipo kuonewa mtu ambapo pia ameshauri kuwa baadhi ya kodi ambazo zinazoweza kuua biashara za watu wenye vipato vya chini ni vema zikaondolewa ili zisiendelee kuwaumiza.

Aidha, Mhe, Nnauye ameahidi kutembelea maeneo ya Viwanja vya ndege ili kuweza kujua baadhi ya bidhaa za kazi za Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa na Watendaji viwanjani hapo zimekuwa zikiishia wapi ili kuondoa malalamiko yanayoelekezwa katika viwanja hivyo.


‘’Niwahakikishieni kwamba nitakwenda mwenyewe katika viwanja vya ndege ili nijue ukweli wa malalamiko yenu kwamba kumekuwa na baadhi ya kazi zenu za sanaa kama vile Uchongaji ambazo zimekuwa zikikamatwa katika baadhi ya viwanja vyetu vya ndege lakini mwisho wa siku hazijulikani zinaishia wapi’’, Alisema, Mhe. Nnauye.

Mhe. Nnauye ameahidi pia kujenga utaratibu wa kutembelea maeneo ya kazi za sanaa mara kwa mara na kwa namna nyingine amewaasa Kampuni ya Quality Group kusaidia kuzitangaza kazi za sanaa za Wachongaji hao kwani wao wameshafungua Duka Maalum ambalo linarahisisha upatikanaji wa bidhaa za sanaa kwa wageni na wenyeji ili kuwasaidia Wachongaji hao nchini.

Sambamba na hayo, Mhe. Nnauye amewashauri Wanachama hao kuunda SACCOS imara ambayo itawasaidia katika kujikwamua kiuchumi kutokana na kazi zao na kuwaahidi kuwatafutia mitaji kwa makubaliano ya kwamba, wanapaswa kuwachagua viongozi waaminifu ambao wanaweza kuongoza vema Saccos hiyo kwa manufaa ya wanachama wote.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA), Bw. Adrian Nyangamalle amepongeza juhudi za Serikali katika kuwasimamia Wasanii kote nchini ambapo ameiomba Serikali pia kuharakisha suala la upatikanaji wa Sera ya Sanaa pamoja na Mfuko wa Sanaa kwa ajili ya Wasanii hao.

‘’Nikuombe Mhe. Waziri kutusaidia kuzishawishi baadhi ya Taasisi na Makampuni nchini kujenga utarataibu wa kuwatembeza wageni wanaokuja nchini katika maeneo ya sanaa ili soko la bidhaa zetu liweze kukukua ndani na nje ya nchi yetu’’, alisema Bw. Nyangamalle.

Chama cha Wasanii na Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA) kilianzishwa mnamo mwaka 1984 na kimesajiliwa kihalali na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) ambapo mbali na majukumu yake kimeweza kuwaandaa na kuwashirikisha Wasanii wa ndani na nje ya nchi pamoja na kutetea Wasanii katika kupata haki zao. 
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment