Waziri asimamisha vigogo TCU


Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof Joyce Ndalichako akijibu maswali bungeni mjini Dodoma jana.

Dodoma. Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amevunja Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na kuwasimamisha kazi mara moja viongozi wake wanne waandamizi kwa tuhuma za kudahili wanafunzi wasiokuwa na sifa.

Mbali ya viongozi hao, Mwenyekiti wa TCU, Awadhi Mawenya naye amesimamishwa kwa kosa la kushindwa kuwachukulia hatua watumishi waliobainika kuwadahili wanafunzi hao.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Profesa Ndalichako alitaja tuhuma zinazowakabili viongozi hao huku akiteua watu wawili kusimamia shughuli za tume hiyo kwa muda.

Profesa Ndalichako ambaye Februari mwaka huu alisitisha mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), George Nyategi na kuwasimamisha kazi wakurugenzi wengine watatu kwa madai ya ukiukwaji wa utoaji wa mikopo pamoja na ucheleweshaji usio na sababu za msingi, alisema Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia kazi za Tume hiyo ikiwa na maana kwamba ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mtendaji mkuu wa taasisi.

Mwingine aliyesimamishwa ni Mkurugenzi wa Ithibati na Uhakiki Ubora, Dk Savinus Maronga kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake wa kusimamia ubora na ithibati ya vyuo vikuu. Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka, Rose Kishweko naye amekumbwa katika kadhia hiyo akidaiwa kudahili wanafunzi wasio na sifa. Pia aliyekuwa akikaimu nafasi hiyo, Kimboka Istambuli naye amesimamishwa.

Walioteuliwa na Profesa Ndalichako kusimamia Tume hiyo kwa muda ni Naibu Makamu Mkuu Chuo Kikuu Ardhi (Utawala na Fedha), Profesa Eleuther ambaye atakuwa Kaimu Katibu Mtendaji na Dk Kokubelwa Moleli ambaye atakuwa Kaimu Mkurugenzi wa Udahili na Nyaraka. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Mratibu wa Idara ya Elimu ya Juu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kilichowaponza

Profesa Ndalichako alisema wanafunzi waliodahiliwa walipata daraja (division) 4.32 lakini wakajiunga na chuo kikuu na kupewa mikopo. Wanafunzi hao wametakiwa kurudisha jumla ya Sh784 milioni huku wakikosa sifa za kusoma ualimu hata wa ngazi ya cheti.

Alisema Chuo Kikuu cha St Joseph kilikuwa kimedahili wanafunzi 424 wasiokuwa na sifa za kujiunga na elimu hiyo lakini pamoja na Serikali kuagiza TCU kuwachukulia hatua waliohusika, hakuna kilichofanyika.

“Serikali iliamua kusitisha masomo ya wanafunzi hao lakini hata hivyo, wizara iliendelea na ukaguzi na mpaka sasa wanafunzi 489 wamebainika kusoma katika chuo hicho bila ya kuwa na sifa za kujiunga na chuo kikuu,” alisema.

Alisema chuo hicho kilibainika kutotoa elimu yenye viwango kiasi cha matawi yake ya Arusha na Songea kufungwa huku wanafunzi waliokuwa wakisoma katika matawi hayo kuhamishiwa katika vyuo vingine.

“Lakini taarifa tuliyoipata kutoka katika Chuo Kikuu cha Dodoma, inasema kuwa kililazimika kuwarudisha mwaka mmoja nyuma wanafunzi waliotoka Chuo Kikuu cha St Joseph mwaka wa tatu kwa kuwa walikuwa hawajui kitu chochote wanachofundishwa,” alisema.

Alisema hali ilikuwa ni hivyohivyo katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) kwani ilibidi waanzishiwe masomo ya ziada (tuition) ili wanafunzi hao waweze kuendana na wenzao huku waliokwenda Mkwawa wakitakiwa kurudia jumla ya masomo 14 kwa kutokuyajua.

Profesa Ndalichako alituma salamu kwa wanafunzi hewa ambao wako vyuoni huku wakiendelea kutafuna fedha za mikopo kuwa dawa yao iko jikoni na imeshachemka akisema atakabiliana nao wakati wowote kwa kushirikiana na Takukuru.
SHARE

  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
  • Image
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment